Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 2:1-13

Mika 2:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wao wanaopanga kutenda maovu wanaolala usiku wakiazimia uovu! Mara tu kunapopambazuka, wanayatekeleza kwani wanao uwezo. Hutamani mashamba na kuyatwaa; wakitaka nyumba, wananyakua. Huwadhulumu wenye nyumba na jamaa zao, huwanyang'anya watu mali zao. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ninapanga kuwaleteeni nyinyi maafa, ambayo kamwe hamtaweza kuyakwepa. Utakuwa wakati mbaya kwenu, wala hamtaweza kwenda kwa maringo. Siku hiyo watu watawasimanga kwa wimbo, watalia na kuomboleza kwa uchungu, wakisema: ‘Tumeangamia kabisa; Mwenyezi-Mungu amechukua nchi yetu, naam, ameiondoa mikononi mwetu. Mashamba yetu amewagawia waliotuteka.’” Kwa hiyo hamtagawiwa sehemu yoyote ya ardhi miongoni mwa watu wake Mwenyezi-Mungu. “Usituhubirie sisi. Mambo kama hayo si ya kuhubiriwa. Sisi hatutakumbwa na maafa! Je, yafaa kusema hivyo, wazawa wa Yakobo? Je, Mwenyezi-Mungu ameacha uvumilivu wake? Je, yeye hufanya mambo kama haya?” Sivyo! Maneno yangu huwafaa watendao mambo mema. Lakini Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: “Nyinyi mnawavamia watu wangu kama adui. Mnawanyang'anya mavazi yao watu watulivu; watu wanaopita kwenda zao bila wasiwasi, na wasio na fikira zozote za vita. Mnawafukuza wake za watu wangu kutoka nyumba zao nzuri; watoto wao mmewaondolea fahari yangu milele. Inukeni mwende zenu! Hapa hamna tena pa kupumzika! Kwa utovu wenu wa uaminifu maangamizi makubwa yanawangojea! Kama mtu angetokea akatamka maneno matupu ya uongo na kusema: ‘Nawatabirieni divai na pombe kwa wingi’, mhubiri wa namna hiyo angependwa na watu hawa! “Lakini kweli nitawakusanya nyote enyi watu wa Yakobo, naam, nitawakusanya enyi Waisraeli mliobaki, niwalete pamoja kama kondoo katika zizi, kama kundi kubwa la kondoo malishoni; nanyi mtakuwa kundi la watu wengi.” Yule atakayetoboa njia atawatangulia, nao watalivunja lango la mji na kutoka nje, watapita na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia; Mwenyezi-Mungu mwenyewe atawatangulia.

Shirikisha
Soma Mika 2

Mika 2:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, sababu wana uwezo mikononi mwao. Nao hutamani mashamba, na kuyanyakua; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi BWANA asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, Sisi tumeangamizwa kabisa; Yeye analibadili fungu la watu wangu; Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu. Kwa hiyo hamtakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa BWANA. Msitabiri, ndivyo watabirivyo; wasiyatabiri mambo haya; lawama hazikomi. Je! Litasemwa neno hili, enyi nyumba ya Yakobo, Roho ya BWANA imepunguzwa? Je! Haya ni matendo yake? Je! Maneno yangu hayamfai yeye aendaye kwa unyofu? Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mnawapokonya joho lililo juu ya nguo za hao wapitao salama bila kutarajia vita. Wanawake wa watu wangu mnawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mnawanyang'anya utukufu wangu milele. Ondokeni, mwende zenu; maana hapa sipo mahali pa raha yenu; kwa sababu ya uchafu mtaangamizwa, naam, kwa maangamizo makubwa sana. Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa. Hakika nitakukusanya, Ee Yakobo, nyote pia; Bila shaka nitawakusanya waliobaki wa Israeli; Nitawaweka pamoja kama kondoo katika zizi; Kama kundi la kondoo katika malisho yao; Watafanya mvumo kwa wingi wa watu; Avunjaye amekwea juu mbele yao; Wamebomoa mahali, wakapita mpaka langoni, Wakatoka nje huko; Mfalme wao naye amepita akiwatangulia, Naye BWANA ametangulia mbele yao.

Shirikisha
Soma Mika 2

Mika 2:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi BWANA asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, Sisi tumeangamizwa kabisa; Yeye analibadili fungu la watu wangu; Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu. Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa BWANA. Msitabiri, ndivyo watabirivyo; wasiyatabiri mambo haya; lawama hazikomi. Je! Litasemwa neno hili, enyi nyumba ya Yakobo, Roho ya BWANA imepunguzwa? Je! Haya ni matendo yake? Je! Maneno yangu hayamfai yeye aendaye kwa unyofu? Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mwaipokonya joho iliyo juu ya nguo za hao wapitao salama kama watu wasiopenda vita. Wanawake wa watu wangu mwawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mwawanyang’anya utukufu wangu milele. Ondokeni, mwende zenu; maana hapa sipo mahali pa raha yenu; kwa sababu ya uchafu mtaangamizwa, naam, kwa maangamizo mazito sana. Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa. Hakika nitakukusanya, Ee Yakobo, nyote pia; Bila shaka nitawakusanya waliobaki wa Israeli; Nitawaweka pamoja kama kondoo wa Bozra; Kama kundi la kondoo kati ya malisho yao; Watafanya mvumo kwa wingi wa watu; Avunjaye amekwea juu mbele yao; Wamebomoa mahali, wakapita mpaka langoni, Wakatoka nje huko; Mfalme wao naye amepita akiwatangulia, Naye BWANA ametangulia mbele yao.

Shirikisha
Soma Mika 2

Mika 2:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ole kwa wale wapangao uovu, kwa wale wapangao hila vitandani mwao! Kunapopambazuka wanalitimiza kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza. Wanatamani mashamba na kuyakamata, pia nyumba na kuzichukua. Wanamlaghai mwanaume nyumba yake, mwanadamu mwenzake urithi wake. Kwa hiyo, BWANA asema: “Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa, ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe. Hamtatembea tena kwa majivuno, kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa. Siku hiyo watu watawadhihaki, watawafanyia mzaha kwa wimbo huu wa maombolezo: ‘Tumeangamizwa kabisa; mali ya watu wangu imegawanywa. Ameninyangʼanya! Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ” Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la BWANA wa kugawanya mashamba kwa kura. Manabii wao husema, “Usitabiri. Usitabiri kuhusu vitu hivi; aibu haitatupata.” Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo: “Je, Roho wa BWANA amekasirika? Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?” “Je, maneno yangu hayamfanyii mema yeye ambaye njia zake ni nyofu? Siku hizi watu wangu wameinuka kama adui. Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita pasipo kujali, kama watu warudio kutoka vitani. Unawahamisha wanawake wa watu wangu kutoka nyumba zao za kupendeza. Unaondoa baraka yangu kwa watoto wao milele. Inuka, nenda zako! Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia, kwa sababu pametiwa unajisi, pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena. Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema, ‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’ angekuwa ndiye nabii anayekubalika na watu hawa! “Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo, Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli. Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi, kama kundi kwenye malisho yake, mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu. Yeye afunguaye njia atawatangulia; watapita kwenye lango na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia, BWANA atakuwa kiongozi.”

Shirikisha
Soma Mika 2