Mika 1:2-7
Mika 1:2-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni enyi watu wote; sikiliza ewe dunia na vyote vilivyomo. Mwenyezi-Mungu anakuja kuwashtaki, Bwana anena kutoka hekalu lake takatifu. Naam! Mwenyezi-Mungu yuaja kutoka makao yake; atashuka na kutembea juu ya vilele vya dunia. Milima itayeyuka chini ya nyayo zake, kama nta karibu na moto; mabonde yatapasuka, kama maji yaporomokayo kwenye mteremko. Haya yote yatatukia kwa sababu ya makosa ya wazawa wa Yakobo, kwa sababu ya dhambi za wazawa wa Israeli. Je, uhalifu wa Yakobo waonekana wapi? Katika mji wake mkuu Samaria! Je, uhalifu wa Yuda waonekana wapi? Katika Yerusalemu kwenyewe! Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mji wa Samaria nitaufanya magofu nyikani, shamba ambalo watu watapanda mizabibu. Mawe yaliyoujenga nitayatupa bondeni, na misingi yake nitaichimbuachimbua. Sanamu zake zote zitavunjwavunjwa, kila kilichochumwa kitateketezwa kwa moto. Vinyago vyake vyote nitaviharibu. Vilirundikwa kutokana na ujira wa malaya, navyo vitatumiwa tena kulipia umalaya.”
Mika 1:2-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye Bwana kutoka hekalu lake takatifu. Kwa maana, angalieni, BWANA anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka. Na hiyo milima itayeyuka chini yake, nayo mabonde yatapasuliwa, kama vile nta iliyo mbele ya moto, kama maji yaliyomwagika katika mteremko. Kwa sababu ya kosa la Yakobo yametokea haya yote, na kwa sababu ya makosa ya nyumba ya Israeli. Nini kosa la Yakobo? Je, silo Samaria? Na nini mahali pa Yuda palipoinuka? Sipo Yerusalemu? Kwa ajili ya hayo nitafanya Samaria kuwa kama chungu katika shamba, na kama miche ya shamba la mizabibu; nami nitayatupa mawe yake bondeni, nami nitaifunua misingi yake. Na sanamu zake zote za kuchonga zitapondwapondwa, na ijara zake zote zitateketezwa kwa moto, na sanamu zake zote nitazifanya ukiwa; kwa kuwa amezikusanya kwa ujira wa kahaba, nazo zitaurudia ujira wa kahaba.
Mika 1:2-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye Bwana kutoka hekalu lake takatifu. Kwa maana, angalieni, BWANA anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka. Na hiyo milima itayeyuka chini yake, nayo mabonde yatapasuliwa, kama vile nta iliyo mbele ya moto, kama maji yaliyomwagika tena kutelemka gengeni. Kwa sababu ya kosa la Yakobo yametokea haya yote, na kwa sababu ya makosa ya nyumba ya Israeli. Nini kosa la Yakobo? Je, silo Samaria? Na nini mahali pa Yuda palipoinuka? Sipo Yerusalemu? Kwa ajili ya hayo nitafanya Samaria kuwa kama chungu katika shamba, na kama miche ya shamba la mizabibu; nami nitayatupa mawe yake bondeni, nami nitaifunua misingi yake. Na sanamu zake zote za kuchonga zitapondwa-pondwa, na ijara zake zote zitateketezwa kwa moto, na sanamu zake zote nitazifanya ukiwa; kwa kuwa amezikusanya kwa ujira wa kahaba, nazo zitaurudia ujira wa kahaba.
Mika 1:2-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote, sikilizeni, ee dunia na wote mliomo, ili BWANA Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu, Bwana kutoka Hekalu lake takatifu. Tazama! BWANA anakuja kutoka mahali pake; anashuka na kukanyaga mahali palipoinuka juu pa dunia. Milima inayeyuka chini yake na mabonde yanagawanyika kama nta mbele ya moto, kama maji yanayotiririka kasi kwenye mteremko. Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo, ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli. Kosa la Yakobo ni lipi? Je, sio Samaria? Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia ni nini? Je, sio Yerusalemu? “Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto, mahali pa kuotesha mizabibu. Nitayamwaga mawe yake katika bonde na kuacha wazi misingi yake. Sanamu zake zote zitavunjwa vipande vipande; zawadi zake zote za Hekalu zitachomwa kwa moto; nitaharibu vinyago vyake vyote. Kwa kuwa alikusanya zawadi zake kutokana na ujira wa kahaba, nazo zitatumika tena kulipa mishahara ya kahaba.”