Mathayo 9:27-34
Mathayo 9:27-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, “Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu alipoingia nyumbani, watu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, “Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?” Nao wakamjibu, “Naam, Bwana.” Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, “Na iwe kwenu kama mnavyoamini.” Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: “Msimwambie mtu yeyote jambo hili.” Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote. Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, “Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!” Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, “Anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya.”
Mathayo 9:27-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu na itendeke kwenu. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote. Na hao walipokuwa wakiondoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.
Mathayo 9:27-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote. Hata hao walipokuwa wakitoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.
Mathayo 9:27-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.” Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Chungeni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote. Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu. Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea, na umati wa watu wakastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.” Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”