Mathayo 9:19-28
Mathayo 9:19-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata. Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, “Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya.” Mama huyo akapona saa ileile. Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaoomboleza, akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka. Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama. Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote. Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, “Mwana wa Daudi, utuhurumie!” Yesu alipoingia nyumbani, watu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, “Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?” Nao wakamjibu, “Naam, Bwana.”
Mathayo 9:19-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu Akaondoka, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana msichana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule msichana akasimama. Habari hizi zikaenea katika nchi ile yote. Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana.
Mathayo 9:19-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote. Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana.
Mathayo 9:19-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye. Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo. Yesu alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote. Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!” Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”