Mathayo 9:18-26
Mathayo 9:18-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali twende umwekee mkono wako naye ataishi.” Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata. Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.” Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, “Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya.” Mama huyo akapona saa ileile. Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaoomboleza, akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka. Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama. Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote.
Mathayo 9:18-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja kiongozi mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Yesu Akaondoka, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana msichana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule msichana akasimama. Habari hizi zikaenea katika nchi ile yote.
Mathayo 9:18-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.
Mathayo 9:18-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, kiongozi wa sinagogi akaingia, akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye. Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.” Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo. Yesu alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.