Mathayo 8:9-13
Mathayo 8:9-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile.
Mathayo 8:9-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule afisa, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona wakati ule ule.
Mathayo 8:9-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile.
Mathayo 8:9-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule.