Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 8:5-17

Mathayo 8:5-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.” Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile. Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.”

Shirikisha
Soma Mathayo 8

Mathayo 8:5-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.” Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.” Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia ndani ya nyumba yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule. Yesu alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na akachukua magonjwa yetu.”

Shirikisha
Soma Mathayo 8