Mathayo 8:14-22
Mathayo 8:14-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.” Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ngambo ya ziwa. Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.”
Mathayo 8:14-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani akiugua homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng'ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.
Mathayo 8:14-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.
Mathayo 8:14-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na akachukua magonjwa yetu.” Yesu alipoona makundi mengi yamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke hadi ngʼambo ya ziwa. Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakakoenda.” Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”