Mathayo 8:1-34
Mathayo 8:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliposhuka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata. Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia na kusema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake. Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.” Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile. Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.” Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ngambo ya ziwa. Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.” Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!” Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa. Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!” Yesu alifika katika nchi ya Wagadara, ngambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita njia hiyo. Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?” Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa. Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.” Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa majini. Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa. Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.
Mathayo 8:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila nenda zako, ukajioneshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao. Na alipoingia Kapernaumu, afisa mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule afisa akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule afisa, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona wakati ule ule. Na Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani akiugua homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng'ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao. Akapanda katika mashua, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa na msukosuko mkuu baharini, hata mashua ikafunikwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii? Naye alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagadara, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wakitoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya wakati wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakila. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakateremka kwa kasi gengeni hadi baharini, wakafa maji. Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke katika nchi yao.
Mathayo 8:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao. Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao. Akapanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii? Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.
Mathayo 8:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makundi ya watu wakamfuata. Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.” Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajioneshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Musa, ili kuwa ushuhuda kwao.” Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.” Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.” Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia ndani ya nyumba yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.” Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule. Yesu alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na akachukua magonjwa yetu.” Yesu alipoona makundi mengi yamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke hadi ngʼambo ya ziwa. Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakakoenda.” Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.” Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.” Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. Ghafula, kukatokea dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!” Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nayo bahari ikatulia kabisa. Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!” Walipofika ngʼambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. Wakapaza sauti wakisema, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?” Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakila. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.” Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji. Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu. Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.