Mathayo 6:7-21
Mathayo 6:7-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba. Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: ‘Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo chakula chetu cha kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea. Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu.’ [ Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] “Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
Mathayo 6:7-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako pia.
Mathayo 6:7-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.
Mathayo 6:7-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba. “Hivi ndivyo mnavyopaswa kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni. Utupatie riziki yetu ya kila siku. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu. Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen].’ Kwa kuwa mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi. “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

