Mathayo 6:16-21
Mathayo 6:16-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
Mathayo 6:16-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako pia.
Mathayo 6:16-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.
Mathayo 6:16-21 Neno (NEN)
“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi. “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.