Mathayo 6:1-6,16-21
Mathayo 6:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
“Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo. “Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata mwandani wako asijue ufanyalo. Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.
Mathayo 6:16-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza. “Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba. Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
Mathayo 6:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kulia; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Mathayo 6:16-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako pia.
Mathayo 6:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Mt 6:16-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.
Mathayo 6:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni. “Hivyo mnapowapa wahitaji, msitangaze hadharani kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi. “Nanyi mnaposali, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupokea thawabu yao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako.
Mathayo 6:16-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi. “Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.