Mathayo 4:23-25
Mathayo 4:23-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. Habari zake zikaenea pande zote za Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: Waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ngambo ya mto Yordani, yalimfuata.
Mathayo 4:23-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila namna waliyokuwa nayo watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa wagonjwa, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Yudea, na ng'ambo ya Yordani.
Mathayo 4:23-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani
Mathayo 4:23-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akazunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Siria, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. Makundi makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea, na kutoka ngʼambo ya Yordani.