Mathayo 4:18-22
Mathayo 4:18-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwaye Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. Basi, akawaambia, “Nifuateni, nami nitawafanya nyinyi wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi, Yesu akawaita, nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata.
Mathayo 4:18-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipoendelea, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwa katika mashua pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakaiacha mashua na baba yao, wakamfuata.
Mathayo 4:18-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
Mathayo 4:18-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. Nao mara moja wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.