Mathayo 4:17-25
Mathayo 4:17-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, “Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekariia!” Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwaye Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani. Basi, akawaambia, “Nifuateni, nami nitawafanya nyinyi wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi, Yesu akawaita, nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata. Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu. Habari zake zikaenea pande zote za Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: Waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote. Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ngambo ya mto Yordani, yalimfuata.
Mathayo 4:17-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipoendelea, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwa katika mashua pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakaiacha mashua na baba yao, wakamfuata. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila namna waliyokuwa nayo watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa wagonjwa, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Yudea, na ng'ambo ya Yordani.
Mathayo 4:17-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani
Mathayo 4:17-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. Nao mara moja wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata. Yesu akazunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Siria, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. Makundi makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea, na kutoka ngʼambo ya Yordani.