Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 28:8-20

Mathayo 28:8-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, lakini wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kupanga njama, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha, wakawaambia, “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” Hivyo basi, wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi hadi leo. Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Kwa sababu hii, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

Shirikisha
Soma Mathayo 28