Mathayo 28:1-7
Mathayo 28:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi. Ghafla kukatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia. Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa. Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, “Nyinyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala. Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka kwa wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.”
Mathayo 28:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la ardhi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; maana amefufuka kama alivyosema. Njooni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.
Mathayo 28:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.
Mathayo 28:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walienda kulitazama kaburi. Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda kwenye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu. Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko.’ Sasa nimekwisha kuwaambia.”