Mathayo 27:26-31
Mathayo 27:26-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe. Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
Mathayo 27:26-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulubiwe. Ndipo askari wa mtawala wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji la miiba, wakaliweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kulia; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampigapiga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulubisha.
Mathayo 27:26-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.
Mathayo 27:26-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe. Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio, na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.