Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 27:1-56

Mathayo 27:1-56 Biblia Habari Njema (BHN)

Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumuua. Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa. Hapo, Yuda, ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu vile vipande thelathini vya fedha. Akawaambia, “Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe.” Lakini wao wakasema, “Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako.” Naye akazitupa zile fedha hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga. Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya hekalu kwa maana ni fedha za damu.” Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Ndio maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu. Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walichukua vipande thelathini vya fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walimtia bei, wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.” Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.” Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno. Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?” Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana. Ilikuwa kawaida wakati wa sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka. Wakati huo kulikuwa na mfungwa aliyejulikana sana, jina lake Baraba. Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwaye Kristo?” Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu. Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe. Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!” Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!” Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!” Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.” Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!” Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe. Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Wakaketi, wakawa wanamchunga. Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.” Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.” Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.

Shirikisha
Soma Mathayo 27

Mathayo 27:1-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa mtawala. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nilikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatuhusu nini sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni fedha ya damu. Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Kwa hiyo shamba lile huitwa shamba la damu hata leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima; wakavitumia kwa kununua shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza. Naye Yesu akasimama mbele ya mtawala; mtawala akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayoshuhudia juu yako? Asimjibu hata neno moja, hata mtawala akastaajabu sana. Basi wakati wa sikukuu, mtawala desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa ajili ya husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi mtawala akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi kati ya hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulubiwe. Akasema, Kwa nini? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulubiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lolote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulubiwe. Ndipo askari wa mtawala wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji la miiba, wakaliweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kulia; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampigapiga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulubisha. Walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la Kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulubisha, waligawana mavazi yake, kwa kupiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko. Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulubiwa pamoja naye, mmoja katika mkono wake wa kulia, na mmoja katika mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang'anyi waliosulubiwa pamoja naye walimshutumu vile vile. Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hadi saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliokuweko, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule afisa, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la ardhi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Shirikisha
Soma Mathayo 27

Mathayo 27:1-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu. Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima; wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza. Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia? Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha. Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa. Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.] Wakaketi, wakamlinda huko. Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. Wakati uo huo wanyang’anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile. Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Shirikisha
Soma Mathayo 27

Mathayo 27:1-56 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, aliyekuwa mtawala Mrumi. Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.” Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.” Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga. Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” Hivyo basi, baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyowekewa na watu wa Israeli, wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.” Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana. Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. Palikuwa na mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza hao watu, “Mnataka niwafungulie yupi: Baraba au Yesu aitwaye Kristo?” Kwa kuwa alitambua kwamba walikuwa wamemkabidhi Yesu kwake kwa ajili ya wivu. Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakashawishi umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe. Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?” Wakajibu, “Baraba.” Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?” Wakajibu wote, “Msulubishe!” Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!” Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya umati wa watu, akasema, “Sina hatia kwa damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!” Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!” Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe. Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio, na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe. Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] Kisha wakaketi, wakamchunga. Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Yesu Mfalme wa Wayahudi. Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao, na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka msalabani.” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo. Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.” Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake. Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi. Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Wanawake wengi walikuwa pale wakitazama kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. Miongoni mwao walikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Shirikisha
Soma Mathayo 27