Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 27:1-14

Mathayo 27:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, aliyekuwa mtawala Mrumi. Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.” Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.” Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga. Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” Hivyo basi, baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyowekewa na watu wa Israeli, wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.” Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.” Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

Shirikisha
Soma Mathayo 27