Mathayo 26:69-74
Mathayo 26:69-74 Biblia Habari Njema (BHN)
Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, “Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Petro akakana mbele ya wote akisema, “Sijui hata unasema nini.” Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Petro akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyo.” Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.” Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, “Simjui mtu huyo!” Mara jogoo akawika.
Mathayo 26:69-74 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Petro alikuwa ameketi nje uani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hadi ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliokuwapo wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara jogoo akawika.
Mathayo 26:69-74 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo.
Mathayo 26:69-74 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.” Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!” Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.” Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!” Papo hapo jogoo akawika.