Mathayo 26:6-13
Mathayo 26:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani. Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Ya nini hasara hii? Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.” Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.”
Mathayo 26:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mwenye ukoma, mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. Wanafunzi wake walipoona, wakakasirika, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamko nami siku zote. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu yake.
Mathayo 26:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma, mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake.
Mathayo 26:6-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula. Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.” Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”