Mathayo 26:44-75
Mathayo 26:44-75 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.” Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika? Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?” Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee. Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa. Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua, lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili, wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’” Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!” Yesu akamwambia, “Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake. Nyinyi mwaonaje?” Wao wakamjibu, “Anastahili kufa!” Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi, wakasema, “Tubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!” Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, “Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Petro akakana mbele ya wote akisema, “Sijui hata unasema nini.” Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Petro akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyo.” Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.” Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, “Simjui mtu huyo!” Mara jogoo akawika. Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Basi, akatoka nje, akalia sana.
Mathayo 26:44-75 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. Ondokeni, twende zetu! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku niliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone ingawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Na baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi katika mkono wa kulia wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. Ndipo wakamtemea mate usoni, wakampiga ngumi; na wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? Na Petro alikuwa ameketi nje uani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hadi ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliokuwapo wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara jogoo akawika. Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya jogoo kuwika, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.
Mathayo 26:44-75 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo. Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.
Mathayo 26:44-75 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!” Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.” Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?” Wakati huo, Yesu akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia. Wale waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia. Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza. Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ” Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya. Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.” Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia alivyokufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wakajibu, “Anastahili kufa.” Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?” Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.” Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!” Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.” Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!” Papo hapo jogoo akawika. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.