Mathayo 26:20-25
Mathayo 26:20-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, “Bwana! Je, ni mimi?” Yesu akajibu, “Anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti. Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.” Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, “Mwalimu! Je, ni mimi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.”
Mathayo 26:20-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Kumi na Wawili. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika bakuli, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
Mathayo 26:20-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
Mathayo 26:20-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!” Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?” Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”