Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 26:1-74

Mathayo 26:1-74 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, “Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe.” Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, kuhani mkuu. Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue. Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu. Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani. Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Ya nini hasara hii? Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha.” Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema. Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko. Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni ambapo hii Habari Njema itahubiriwa, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.” Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu, akawaambia, “Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?” Wakamhesabia vipande thelathini vya fedha; na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti. Siku ya kwanza kabla ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?” Yeye akawajibu, “Nendeni mjini kwa mwanamume fulani, mkamwambie: ‘Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.’” Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka. Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, “Bwana! Je, ni mimi?” Yesu akajibu, “Anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti. Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa.” Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, “Mwalimu! Je, ni mimi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.” Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akamshukuru Mungu, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ni mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akawapa akisema, “Kunyweni nyote; maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi. Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni. Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu wa leo, nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: ‘Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.’ Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya.” Petro akamwambia Yesu, “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe.” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Petro akamwambia, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.” Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. Hapo akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.” Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.” Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.” Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika? Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?” Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu, walikokusanyika waalimu wa sheria na wazee. Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa. Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumuua, lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili, wakasema, “Mtu huyu alisema: ‘Ninaweza kuliharibu hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’” Kuhani mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!” Yesu akamwambia, “Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Hapo, kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake. Nyinyi mwaonaje?” Wao wakamjibu, “Anastahili kufa!” Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi, wakasema, “Tubashirie basi, wewe Kristo; ni nani amekupiga!” Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, “Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Petro akakana mbele ya wote akisema, “Sijui hata unasema nini.” Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Petro akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyo.” Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha.” Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, “Simjui mtu huyo!” Mara jogoo akawika.

Shirikisha
Soma Mathayo 26

Mathayo 26:1-74 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulubiwe. Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua. Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia miongoni mwa watu. Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mwenye ukoma, mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. Wanafunzi wake walipoona, wakakasirika, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamko nami siku zote. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu yake. Wakati huo mmoja wa wale Kumi na Wawili, jina lake Yuda Iskarioti, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Katika siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Kumi na Wawili. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika bakuli, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema. Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Kuyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda katika mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniondokee; lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho iko radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniondokee nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yalijawa na usingizi. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. Ondokeni, twende zetu! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku niliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone ingawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Na baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi katika mkono wa kulia wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. Ndipo wakamtemea mate usoni, wakampiga ngumi; na wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? Na Petro alikuwa ameketi nje uani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hadi ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliokuwapo wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara jogoo akawika.

Shirikisha
Soma Mathayo 26

Mathayo 26:1-74 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulibiwe. Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua. Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma, mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake. Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema. Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo.

Shirikisha
Soma Mathayo 26

Mathayo 26:1-74 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.” Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. Wakapanga kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.” Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula. Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.” Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.” Kisha mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alienda kwa viongozi wa makuhani na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu. Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” Hivyo wanafunzi wakafanya vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!” Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?” Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.” Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.” Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni. Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’ Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.” Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.” Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo. Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake hadi kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.” Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!” Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.” Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?” Wakati huo, Yesu akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia. Wale waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia. Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza. Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ” Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” Lakini Yesu akakaa kimya. Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.” Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia alivyokufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wakajibu, “Anastahili kufa.” Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?” Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.” Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.” Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!” Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.” Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!” Papo hapo jogoo akawika.

Shirikisha
Soma Mathayo 26