Mathayo 25:31-46
Mathayo 25:31-46 Biblia Habari Njema (BHN)
“Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu. Mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto. “Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, ‘Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’ Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme ‘Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji? Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika? Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?’ Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.’ “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji. Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.’ “Hapo nao watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukukuhudumia?’ Naye atawajibu, ‘Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.’ Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uhai wa milele.”
Mathayo 25:31-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote yatakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo katika mkono wake wa kulia, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko katika mkono wake wa kulia, Njooni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nilikuwa na njaa, mkanipa chakula; nilikuwa na kiu, mkaninywesha; nilikuwa mgeni, mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nilikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona ukiwa na njaa, tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona ukiwa mgeni, tukakukaribisha, au ukiwa uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona ukiwa mgonjwa, au ukiwa kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko katika mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nilikuwa na njaa, msinipe chakula; nilikuwa na kiu, msininyweshe; nilikuwa mgeni, msinikaribishe; nilikuwa uchi, msinivike; nilikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe ukiwa na njaa, au ukiwa na kiu, au ukiwa mgeni, au ukiwa uchi, au ukiwa mgonjwa, au ukiwa kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Mathayo 25:31-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Mathayo 25:31-46 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi kwenye kiti cha enzi cha utukufu wake. Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto. “Ndipo Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, nilikuwa uchi mkanivisha nguo, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’ “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvisha nguo? Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’ “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmoja wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’ “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika wake. Kwa maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu nanyi hamkuninywesha, nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi nanyi hamkunivisha nguo, nilikuwa mgonjwa nanyi hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’ “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’ “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi hamkumtendea mmoja wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’ “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”