Mathayo 23:16-22
Mathayo 23:16-22 Biblia Habari Njema (BHN)
“Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika. Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika. Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu? Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake. Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake. Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.
Mathayo 23:16-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga kwa kiapo. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga kwa kiapo. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
Mathayo 23:16-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
Mathayo 23:16-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’ Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’ Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu? Basi, mtu anayeapa kwa madhabahu, anaapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake. Naye mtu anayeapa kwa Hekalu, anaapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake. Naye anayeapa kwa mbingu, anaapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye anayeketi kwenye kiti hicho.