Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 21:33-44

Mathayo 21:33-44 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’ Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?” Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.” Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? ‘Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!’ “Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.” Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda” (taz. Luka 20:18).

Shirikisha
Soma Mathayo 21

Mathayo 21:33-44 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo la kukamulia zabibu ndani yake, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri hadi nchi nyingine. Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake. “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. Kisha akawatuma watumishi wengine kwao, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’ “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua. “Basi huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?” Wakamjibu, “Kwa hasira kuu, atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.” Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la kushangaza machoni petu’? “Kwa hiyo ninawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

Shirikisha
Soma Mathayo 21