Mathayo 21:23-46
Mathayo 21:23-46 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?” Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.” Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. “Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi. Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini. Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.” Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.” Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali. Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake. Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe. Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile. Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’ Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’ Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?” Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.” Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? ‘Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!’ “Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.” Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda” (taz. Luka 20:18). Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao. Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.
Mathayo 21:23-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda haya. Lakini mnaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu. Naye akajibu akasema, Siendi, lakini baadaye akatubu akaenda. Akamwendea yule wa pili, akamwambia vile vile. Naye akajibu akasema, Naenda Bwana; lakini hakuenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa kwanza. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini. Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye shamba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa kuvuna matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni la ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande; naye yeyote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Mathayo 21:23-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya. Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini. Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Mathayo 21:23-46 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha, wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka haya?” Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. Je, ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.” Hivyo basi wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya. “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitaenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda. “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine, akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitaenda, bwana,’ lakini hakuenda. “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?” Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.” Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki. “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo la kukamulia zabibu ndani yake, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri hadi nchi nyingine. Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake. “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. Kisha akawatuma watumishi wengine kwao, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’ “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua. “Basi huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?” Wakamjibu, “Kwa hasira kuu, atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.” Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la kushangaza machoni petu’? “Kwa hiyo ninawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.” Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.