Mathayo 21:1-7
Mathayo 21:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji,’ naye atawaachieni mara.” Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie: “Uambieni mji wa Siyoni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda.” Hivyo, wale wanafunzi walikwenda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake.
Mathayo 21:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Nendeni katika kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; naye atawatuma mara moja. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwanapunda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwanapunda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.
Mathayo 21:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.
Mathayo 21:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.” Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mpole, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’” Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake.