Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 18:21-34

Mathayo 18:21-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, “Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?” Yesu akamjibu, “Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba. Ndiyo maana ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake. Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta 10,000. Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru auzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, ‘Unisubiri nami nitakulipa deni lote’. Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake. “Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha dinari 100. Akamkamata, akamkaba koo akisema, ‘Lipa deni lako!’ Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, ‘Unisubiri nami nitakulipa’. Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni. “Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia. Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?’ “Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote.

Shirikisha
Soma Mathayo 18

Mathayo 18:21-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha Petro akamwendea Yesu na kumuuliza, “Bwana, ni mara ngapi nimsamehe ndugu yangu akinikosea? Hadi mara saba?” Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. “Kwa hiyo ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta elfu kumi aliletwa kwake. Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa. “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake. “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’ “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia. “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe hadi atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

Shirikisha
Soma Mathayo 18