Mathayo 18:1-9
Mathayo 18:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Ni nani aliye mkubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni?” Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao, kisha akasema, “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. “Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. Na jicho lako likikukosesha, lingoe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili.
Mathayo 18:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekezaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika Jehanamu ya moto.
Mathayo 18:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.
Mathayo 18:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni?” Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika ufalme wa mbinguni. Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika ufalme wa mbinguni. “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. “Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari. “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha. Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa Jehanamu.