Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 12:22-32

Mathayo 12:22-32 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo watu wakamletea Yesu mtu mmoja kipofu na ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata akaweza kusema na kuona. Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, “Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, “Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? Nyinyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake. “Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao.

Shirikisha
Soma Mathayo 12

Mathayo 12:22-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.” Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekuja juu yenu. “Au tena, mtu anawezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali yake. “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

Shirikisha
Soma Mathayo 12