Mathayo 12:14-21
Mathayo 12:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, ili yale aliyosema Mungu kwa njia ya nabii Isaya yatimie: “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.”
Mathayo 12:14-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hadi ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Mathayo 12:14-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Mathayo 12:14-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Yesu. Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao, akiwakataza wasiseme yeye ni nani, ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema: “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. Hatagombana wala kupaza sauti, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, hadi atakapoifanya haki ishinde. Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”