Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 12:1-37

Mathayo 12:1-37 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. Au je, hamjasoma katika kitabu cha sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja sheria hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko hekalu. Kama tu mngejua maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma wala si tambiko,’ hamngewahukumu watu wasio na hatia. Maana Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.” Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akawaambia, “Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? Lakini, mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, ili yale aliyosema Mungu kwa njia ya nabii Isaya yatimie: “Tazama mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. Kwake yeye mataifa yatakuwa na matumaini.” Hapo watu wakamletea Yesu mtu mmoja kipofu na ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata akaweza kusema na kuona. Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, “Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, “Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? Nyinyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake. “Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mazuri; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali nyinyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. “Basi, nawaambieni, siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. Maana kwa maneno yako utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako utahukumiwa kuwa na hatia.”

Shirikisha
Soma Mathayo 12

Mathayo 12:1-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato pasipo kupata hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Ili wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato. Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hadi ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia. Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yoyote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu yeyote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazawa wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.

Shirikisha
Soma Mathayo 12

Mathayo 12:1-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato. Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili. Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia. Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.

Shirikisha
Soma Mathayo 12

Mathayo 12:1-37 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.” Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu. Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?” Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. Lakini Mafarisayo wakatoka nje na kupanga njama ya kumuua Yesu. Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi walimfuata, naye akawaponya wote waliokuwa wagonjwa miongoni mwao, akiwakataza wasiseme yeye ni nani, ili neno lililonenwa na nabii Isaya litimie, aliposema: “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. Hatagombana wala kupaza sauti, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, hadi atakapoifanya haki ishinde. Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.” Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?” Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.” Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekuja juu yenu. “Au tena, mtu anawezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali yake. “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao. “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa maelezo kuhusu kila neno walilonena lisilo la maana. Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

Shirikisha
Soma Mathayo 12