Malaki 3:1-4
Malaki 3:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Tazama, namtuma mjumbe wangu anitangulie kunitayarishia njia. Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafla. Mjumbe mnayemtazamia kwa hamu kubwa atakuja na kutangaza agano langu.” Lakini ni nani atakayestahimili siku hiyo atakapokuja? Ni nani atakayesimama kustahimili atakapotokea? Yeye ni kama moto mkali usafishao chuma; ni kama sabuni ya dobi. Yeye atakuja kuhukumu kama mtu asafishaye na kutakasa fedha. Atawasafisha wazawa wa Lawi, kama mtu afuavyo dhahabu au fedha, mpaka wamtolee Mwenyezi-Mungu tambiko zinazokubalika. Hivyo, tambiko za watu wa Yuda na wa Yerusalemu zitampendeza Mwenyezi-Mungu kama za watu wa kale; kama katika miaka ya zamani.
Malaki 3:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijia katika hekalu lake ghafla; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea BWANA dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za BWANA, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
Malaki 3:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea BWANA dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za BWANA, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
Malaki 3:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Angalieni, nitamtuma mjumbe wangu, atakayeiandaa njia mbele yangu. Ndipo ghafula Bwana mnayemtafuta atakuja hekaluni mwake. Mjumbe wa agano, ambaye mnamwonea shauku, atakuja,” asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayeweza kustahimili hiyo siku ya kuja kwake? Ni nani awezaye kusimama atakapotokea? Kwa kuwa atakuwa kama moto wa mfua fedha au kama sabuni ya mfua nguo. Ataketi kama mfuaji na asafishaye fedha. Atawatakasa Walawi, naye atawasafisha kama dhahabu na fedha. Kisha BWANA atakuwa na watu watakaoleta sadaka katika haki, nazo sadaka za Yuda na Yerusalemu zitakubalika kwa BWANA, kama katika siku zilizopita, kama katika miaka ya zamani.