Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Malaki 3:1-10

Malaki 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Tazama, namtuma mjumbe wangu anitangulie kunitayarishia njia. Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafla. Mjumbe mnayemtazamia kwa hamu kubwa atakuja na kutangaza agano langu.” Lakini ni nani atakayestahimili siku hiyo atakapokuja? Ni nani atakayesimama kustahimili atakapotokea? Yeye ni kama moto mkali usafishao chuma; ni kama sabuni ya dobi. Yeye atakuja kuhukumu kama mtu asafishaye na kutakasa fedha. Atawasafisha wazawa wa Lawi, kama mtu afuavyo dhahabu au fedha, mpaka wamtolee Mwenyezi-Mungu tambiko zinazokubalika. Hivyo, tambiko za watu wa Yuda na wa Yerusalemu zitampendeza Mwenyezi-Mungu kama za watu wa kale; kama katika miaka ya zamani. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kisha nitawakaribia ili kuwahukumu. Sitasita kutoa ushahidi dhidi ya wachawi, wazinzi, watoa ushahidi wa uongo, wanaowapunja waajiriwa, wanaowadhulumu wageni na wale wasionicha mimi. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, mimi sibadiliki. Lakini nyinyi, nyinyi wazawa wa Yakobo hamjatoweka bado. Tangu wakati wa wazee wenu, mmezidharau kanuni zangu wala hamkuzifuata. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nasema: Nirudieni, nami nitawageukieni. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tutakurudia namna gani?’ Nami nawaulizeni, Je, ni sawa mtu kumdanganya Mungu? La! Lakini nyinyi mnanidanganya! Walakini nyinyi mwauliza: ‘Tunakudanganya kwa namna gani?’ Naam! Mnanidanganya kuhusu zaka na tambiko zenu. Nyinyi na taifa lenu lote mmelaaniwa kwa sababu ya kunidanganya. Leteni ghalani mwangu zaka yote, ili nyumbani mwangu kuwe na chakula cha kutosha. Kisha mwaweza kunijaribu. Nijaribuni namna hiyo nanyi mtaona kama sitayafungua madirisha ya mbinguni na kuwatiririshia baraka tele.

Shirikisha
Soma Malaki 3

Malaki 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijia katika hekalu lake ghafla; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea BWANA dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za BWANA, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani. Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami sitasita kutoa ushahidi juu ya wachawi; na juu ya wazinzi, na juu ya waapao kwa uongo; juu ya wamwoneao mwajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi. Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo. Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.

Shirikisha
Soma Malaki 3

Malaki 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea BWANA dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za BWANA, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani. Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi. Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo. Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.

Shirikisha
Soma Malaki 3

Malaki 3:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Angalieni, nitamtuma mjumbe wangu, atakayeiandaa njia mbele yangu. Ndipo ghafula Bwana mnayemtafuta atakuja hekaluni mwake. Mjumbe wa agano, ambaye mnamwonea shauku, atakuja,” asema BWANA wa majeshi. Lakini ni nani atakayeweza kustahimili hiyo siku ya kuja kwake? Ni nani awezaye kusimama atakapotokea? Kwa kuwa atakuwa kama moto wa mfua fedha au kama sabuni ya mfua nguo. Ataketi kama mfuaji na asafishaye fedha. Atawatakasa Walawi, naye atawasafisha kama dhahabu na fedha. Kisha BWANA atakuwa na watu watakaoleta sadaka katika haki, nazo sadaka za Yuda na Yerusalemu zitakubalika kwa BWANA, kama katika siku zilizopita, kama katika miaka ya zamani. “Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowadhulumu wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema BWANA wa majeshi. “Mimi BWANA sibadiliki. Kwa hiyo ninyi, enyi uzao wa Yakobo, hamjaangamizwa. Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema BWANA wa majeshi. “Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’ “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi. “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’ “Mnaniibia zaka na dhabihu. Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema BWANA wa majeshi, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi hata mkose nafasi ya kutosha.

Shirikisha
Soma Malaki 3

Malaki 3:1-10

Malaki 3:1-10 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima