Malaki 2:14-16
Malaki 2:14-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnauliza, “Mbona sasa hazikubali?” Mwenyezi-Mungu hazikubali kwa sababu anajua wazi kuwa umeivunja ahadi yako kwa mke wa ujana wako. Umekosa uaminifu kwake ingawa uliahidi mbele ya Mungu kwamba ungekuwa mwaminifu kwake. Je, Mungu hakuwafanya nyote wawili muwe mwili mmoja na roho moja? Je, alikusudia nini alipofanya hayo? Yamkini alikusudia tuzae watoto ambao watamcha yeye. Kwa hiyo, hakikisheni kuwa hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema: “Ninachukia talaka. Ninachukia mmoja wenu anapomtendea mkewe ukatili huo. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja wenu anayekosa uaminifu kwa mkewe.”
Malaki 2:14-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, ingawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzawa mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
Malaki 2:14-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako. Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
Malaki 2:14-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu BWANA ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa. Je, BWANA hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake. “Ninachukia kuachana,” asema BWANA, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema BWANA wa majeshi. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.