Malaki 1:1-5
Malaki 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Kauli ya Mwenyezi-Mungu iliyomjia Malaki awaambie Waisraeli. Mwenyezi-Mungu asema: “Daima nimewapenda nyinyi”. Lakini watu wa Israeli wanauliza, “Umetupendaje?” Naye Mwenyezi-Mungu asema: “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nilimpenda Yakobo nikamchukia Esau. Nimeiharibu nchi ya milima ya Esau ambayo ni urithi wake, nikawaachia mbwamwitu wa jangwani. Nao wazawa wa Esau, yaani Waedomu, wanasema kwamba ingawa miji yao imeharibiwa, watajenga upya magofu yake. Lakini, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba wanaweza kuijenga upya, lakini mimi nitaibomolea mbali. Watu watawaita, ‘Taifa ovu ambalo Mwenyezi-Mungu amelikasirikia milele.’ Nanyi mtakapoyaona hayo kwa macho yenu, mtatambua na kusema: ‘Ukuu wa Mwenyezi-Mungu wafika hata nje ya mipaka ya nchi ya Israeli.’”
Malaki 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo wa neno la BWANA kwa Israeli kwa mkono wa Malaki Nimewapenda ninyi, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema BWANA; ila nimempenda Yakobo; bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani. Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwapondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; BWANA wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha; na watu watawaita, Mpaka wa uovu, na, Watu ambao BWANA anawaghadhabikia milele. Na macho yenu ninyi yataona, nanyi mtasema, BWANA ndiye mkuu hata katika nje ya mipaka ya Israeli.
Malaki 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo wa neno la BWANA kwa Israeli kwa mkono wa Malaki Nimewapenda ninyi, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema BWANA; ila nimempenda Yakobo; bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani. Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwa-pondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; BWANA wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha; na watu watawaita, Mpaka wa uovu, na, Watu ambao BWANA anawaghadhabikia milele. Na macho yenu ninyi yataona, nanyi mtasema, BWANA ndiye mkuu kupita mpaka wa Israeli.
Malaki 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la unabii: Neno la BWANA kwa Israeli kupitia kwa Malaki. BWANA asema, “Nimewapenda ninyi. “Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ” BWANA asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo, lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya nchi yake ya vilima kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.” Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondapondwa, tutajenga upya magofu.” Lakini hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya BWANA. Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘BWANA ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’