Luka 20:27-38
Luka 20:27-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Masadukayo, ambao husema kwamba wafu hawafufuki, wakamjia Yesu, wakasema: “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu ya mtu fulani akifa na kumwacha mjane wake bila watoto, ni lazima ndugu yake amchukue huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Sasa, wakati mmoja kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza alioa na baadaye akafa bila kuacha mtoto. Yule ndugu wa pili akamwoa yule mjane, naye pia akafa; na ndugu wa tatu vilevile. Mambo yakawa yaleyale kwa wote saba – wote walikufa bila kuacha watoto. Mwishowe akafa pia yule mwanamke. Je, siku wafu watakapofufuliwa, mama huyo atakuwa mke wa nani? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawaambia, “Watu wa nyakati hizi huoa na kuolewa; lakini wale ambao Mungu atawawezesha kushiriki ule wakati wa ufufuo, hawataoa wala kuolewa. Ama hakika, hawawezi kufa tena, kwa sababu watakuwa kama malaika, na ni watoto wa Mungu kwa vile wamefufuliwa katika wafu. Lakini, kwamba kuna kufufuka kutoka kwa wafu, hata Mose alithibitisha jambo hilo katika Maandiko Matakatifu. Katika sehemu ya Maandiko Matakatifu juu ya kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto, anamtaja Bwana kama Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa wale walio hai; maana kwake wote wanaishi.”
Luka 20:27-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura ya Kichaka, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa maana kwake wote wanaishi.
Luka 20:27-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.
Luka 20:27-38 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. Basi kulikuwa na ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto. Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto, naye wa tatu pia akamwoa. Vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke, na wote wakafa pasipo yeyote kupata mtoto. Mwishowe, yule mwanamke naye akafa. Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?” Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi. Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo. Hata Musa alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Bwana, ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’ Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.”