Luka 14:7-24
Luka 14:7-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano: “Kama mtu akikualika harusini, usiketi mahali pa heshima, isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe; na mwenyeji wenu nyinyi wawili atakuja na kukuambia: ‘Mwachie huyu nafasi.’ Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho. Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akuambie: ‘Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.’ Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe. Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa na anayejishusha, atakwezwa.” Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, “Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri wasije nao wakakualika, nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea. Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu, nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka.” Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, “Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika ufalme wa Mungu.” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akawaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake akawaambie walioalikwa, ‘Njoni, kila kitu ni tayari.’ Lakini wote, mmoja baada ya mwingine, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: ‘Nimenunua shamba, na hivyo sina budi niende kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.’ Mwingine akasema: ‘Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima, sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.’ Na mwingine akasema: ‘Nimeoa kwa hiyo siwezi kuja.’ Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: ‘Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na vilema wengine.’ Baadaye, mtumishi huyo akasema: ‘Bwana, mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.’ Yule bwana akamwambia mtumishi: ‘Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae. Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.’”
Luka 14:7-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika nawe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki. Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njooni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akamwambia Bwana wake kuhusu mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hakuna hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
Luka 14:7-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki. Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.
Luka 14:7-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu: “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe. Mkifanya hivyo, yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa. Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule aliyekualika atakapokuona, atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote. Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.” Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umepata malipo. Bali unapoandaa karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu, nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.” Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya ufalme wa Mungu!” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’ “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’ “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninaenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ “Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’ “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’ “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’ “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyo nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ijae. Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”