Luka 13:1-32
Luka 13:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko. Naye Yesu akawaambia, “Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo? Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu mtaangamia kama wao. Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu, wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu? Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao.” Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini shambani mwake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja. Basi, akamwambia mfanyakazi wake: ‘Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, bila kupata chochote. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?’ Lakini yeye akamjibu: ‘Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea. Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata.’” Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato. Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima. Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, “Mama, umeponywa ugonjwa wako.” Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu. Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya huyo mama siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu waliokusanyika pale, “Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato.” Hapo Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato? Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?” Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda. Yesu akauliza: “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini? Ni kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota na kuwa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake.” Tena akauliza: “Nitaulinganisha ufalme wa Mungu na nini? Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga madebe mawili na nusu kisha unga wote ukaumuka.” Yesu aliendelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri. Mtu mmoja akamwuliza, “Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?” Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Nyinyi mtasimama nje na kuanza kubisha mlango mkisema: ‘Bwana, tufungulie mlango.’ Lakini yeye atawajibu: ‘Sijui mmetoka wapi.’ Nanyi mtaanza kumwambia: ‘Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.’ Lakini yeye atasema: ‘Sijui nyinyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.’ Ndipo kutakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo na manabii wote wapo katika ufalme wa Mungu, lakini nyinyi wenyewe mmetupwa nje! Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini na kukaa kwenye karamu katika ufalme wa Mungu. Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho.” Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua.” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: ‘Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.’
Luka 13:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii nimekuja kutafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate. Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Abrahamu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye. Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia. Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Abrahamu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho. Saa ile ile Mafarisayo kadhaa walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilisha kazi yangu.
Luka 13:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate. Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye. Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia. Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho. Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.
Luka 13:1-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa. Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo kama hicho walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote? La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo. Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote walioishi Yerusalemu? Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.” Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja. Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’ “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uuache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea. Nao ukizaa matunda mwaka ujao, vyema! La sivyo, uukate.’ ” Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na nane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” Yesu alipomwekea mikono yake, akasimama wima mara moja, akaanza kumtukuza Mungu. Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia umati ule wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.” Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti ya Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na nane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?” Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya. Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini? Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti, nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.” Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha ufalme wa Mungu na nini? Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.” Yesu akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?” Yesu akawaambia, “Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza. Mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’ “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’ “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’ “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’ “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje. Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika ufalme wa Mungu. Tazama, kuna walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.” Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’