Luka 1:57-66
Luka 1:57-66 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Luka 1:57-66 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya Yudea yenye milima. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Luka 1:57-66 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Luka 1:57-66 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye. Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake. Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.” Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.” Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu. Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima ya Yudea watu walikuwa wakinena kuhusu mambo haya yote. Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.