Walawi 7:1-38
Walawi 7:1-38 Biblia Habari Njema (BHN)
“Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuondoa hatia. Sadaka hiyo ni takatifu kabisa. Mnyama wa sadaka ya kuondoa hatia atachinjiwa mahali wanapochinjiwa wanyama wa sadaka za kuteketezwa, na damu yake itarashiwa madhabahu pande zake zote. Mafuta yake yote: Mafuta ya mkia na yale yanayofunika matumbo yatatolewa na kuteketezwa pamoja na zile figo mbili pamoja na mafuta yake na ile sehemu bora ya ini. Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni sadaka ya kuondoa hatia. Wanaoruhusiwa kula sadaka hiyo ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao; ni sadaka takatifu kabisa. Italiwa katika mahali patakatifu. Sheria ni moja kuhusu sadaka ya kuondoa hatia na sadaka ya kuondoa dhambi: Kuhani anayefanya ibada ya upatanisho ndiye atakayeichukua. Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa ya mtu yeyote, atachukua ngozi ya mnyama aliyetolewa. Sadaka yoyote ya nafaka iliyookwa jikoni au katika sufuria au katika kikaango itakuwa mali ya kuhani anayeitoa. Kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au kavu, itakuwa ya wazawa wa Aroni, na wote wagawiwe kwa sawa. “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka za amani ambazo mtu aweza kumtolea Mwenyezi-Mungu. Ikiwa mtu anatoa sadaka hiyo ya kumshukuru Mungu, basi, ataitoa pamoja na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyopakwa mafuta, mikate myembamba iliyopakwa mafuta na maandazi ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Pamoja na sadaka hiyo yake ya amani ya kumshukuru Mungu, ataleta maandazi yaliyotiwa chachu. Kutokana na maandazi hayo, atamtolea Mwenyezi-Mungu andazi moja kutoka kila sadaka; maandazi hayo yatakuwa yake kuhani anayeirashia madhabahu damu ya sadaka za amani. Nyama ya sadaka hiyo ya amani ya kumshukuru Mungu italiwa siku hiyohiyo inapotolewa; hataacha hata sehemu yake hadi asubuhi. Lakini kama sadaka hiyo ya amani ni ya nadhiri au ya hiari, italiwa siku hiyohiyo inapotolewa na sehemu nyingine yaweza kuliwa kesho yake. Lakini nyama yoyote ya sadaka hiyo inayobaki hadi siku ya tatu itateketezwa. Tena nyama yoyote ya sadaka ya amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitapokelewa kwa faida yake mtu aliyeitoa. Nyama hiyo ni chukizo na mtu atakayeila atawajibika kwa uovu wake. “Nyama yoyote inayogusa kitu najisi isiliwe. Nyama hiyo itateketezwa kwa moto. Wote walio safi wanaweza kula nyama iliyotolewa sadaka ya amani kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini mtu yeyote aliye najisi, akila nyama hiyo, atatengwa na watu wake. Mtu yeyote anayegusa kitu chochote kilicho najisi, au kitu najisi cha mtu, au mnyama aliye najisi, au kitu chochote najisi ambacho ni chukizo, akila nyama ya sadaka ya amani aliyotolewa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atatengwa na watu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Msile mafuta ya ng'ombe au ya kondoo au ya mbuzi. Mafuta ya mnyama yoyote aliyekufa mwenyewe au ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini yaweza kuwekwa kwa matumizi mengine, lakini kamwe msiyale. Mtu yeyote akila mafuta ya mnyama aliyetolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto, atatengwa na watu wake. Tena, kamwe msile damu yoyote ile, iwe ya ndege au ya mnyama mahali popote mnapoishi. Mtu yeyote akila damu yoyote, atatengwa na watu wake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Mtu yeyote akitoa sadaka ya amani, atampa Mwenyezi-Mungu sehemu ya sadaka hiyo. Atamletea kwa mikono yake mwenyewe kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Ataleta mafuta yake pamoja na kidari ambacho atafanya nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Kuhani atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Aroni na wanawe makuhani. Mguu wa kulia wa nyuma wa mnyama wa sadaka zenu za amani mtampa kuhani. Mguu huo utakuwa mali ya kuhani aliye mzawa wa Aroni anayetoa damu ya sadaka za amani na mafuta yake. Mwenyezi-Mungu amewaagiza watu wa Israeli watenge kidari hicho na mguu huo wa mnyama wa sadaka zao za amani, wampe kuhani Aroni na wazawa wake, maana sehemu hiyo wamewekewa hao makuhani milele. Hiyo ndiyo sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Aroni na wanawe kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto, tangu siku walipotawazwa kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu. Walipowekwa wakfu kwa kupakwa mafuta, Mwenyezi-Mungu aliamuru Waisraeli wawape sehemu hiyo ya sadaka; hiyo itakuwa daima haki yao.” Basi, hayo ndiyo maagizo kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya kuondoa dhambi, sadaka ya kuondoa hatia, kuhusu kuwekwa wakfu na kuhusu sadaka ya amani. Mwenyezi-Mungu alimpa Mose amri hizi mlimani Sinai siku ile alipowaamuru Waisraeli wamletee sadaka zao, kule jangwani Sinai.
Walawi 7:1-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na sheria ya hiyo sadaka ya hatia ni hii; ni takatifu sana. Wataichinja sadaka ya hatia pale pale waichinjapo sadaka ya kuteketezwa; na damu yake atainyunyiza katika madhabahu pande zote. Katika sadaka hiyo atasongeza mafuta yake yote; yaani, mkia wake wenye mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na figo zake mbili, hayo yote atayaondoa; na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kuwa dhabihu kwa BWANA kwa njia ya moto; ni sadaka ya hatia. Kila mwanamume miongoni mwa makuhani atakula katika sadaka hiyo; italiwa katika mahali patakatifu; ni takatifu sana. Kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo, na sadaka ya hatia ni vivyo hivyo; sheria yake ni moja; huyo kuhani afanyaye upatanisho kwayo, ndiye atakayekuwa nayo. Tena kuhani atakayesongeza sadaka ya kuteketezwa ya mtu awaye yote, huyo kuhani atatwaa awe nayo ngozi ya huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa aliyemsongeza. Na kila sadaka ya unga iliyookwa mekoni, na yote yaliyoandaliwa chunguni, au kaangoni, yote yatakuwa ya huyo kuhani aliyeyasongeza. Na kila sadaka ya unga, kama umeandaliwa na mafuta, au kama ni mkavu, watautwaa wana wote wa Haruni kuutumia, kila mtu sawasawa. Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa BWANA, ni hii. Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta. Ataleta matoleo yake, pamoja na mikate iliyotiwa chachu, na pamoja na sadaka zake za amani, kwa ajili ya shukrani. Na katika hayo atasongeza kimoja katika kila toleo kiwe sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA; itakuwa ni ya kuhani atakayeinyunyiza hiyo damu ya sadaka za amani. Na hiyo nyama ya sadaka zake za amani zilizochinjwa kwa ajili ya shukrani italiwa siku iyo hiyo ya matoleo yake; asisaze yoyote hata asubuhi. Lakini ikiwa hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa; lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto. Tena kama nyama yoyote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake. Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila; lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu chochote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yoyote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yoyote, ya ng'ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi. Tena mafuta ya mnyama afaye mwenyewe, na mafuta ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, mna ruhusa kuyatumia kwa matumizi mengine; lakini msiyale kamwe. Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa BWANA kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake. Tena msiile damu yoyote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote. Mtu yeyote alaye damu, mtu huyo atatupiliwa mbali na watu wake. BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa BWANA, atamletea BWANA matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani; mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atavileta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya BWANA. Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na wanawe. Mguu wa nyuma wa upande wa kulia mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka kwa hizo sadaka zenu za amani. Kati ya wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kulia kuwa sehemu yake. Kwa maana, hicho kidari cha kutikiswa, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli. Hii ndiyo sehemu ya Haruni, na sehemu ya wanawe, katika kutiwa mafuta kwao, katika hizo dhabihu zisongezwazo kwa BWANA kwa njia ya moto, siku hiyo aliyowaweka ili wamtumikie BWANA katika kazi ya ukuhani; sehemu ambayo BWANA aliagiza wapewe na wana wa Israeli, siku hiyo aliyowatia mafuta. Ni haki yao ya milele katika vizazi vyao vyote. Sheria ya sadaka ya kuteketezwa ni hii, na ya sadaka ya unga, na ya sadaka ya dhambi, na ya sadaka ya hatia, na ya kuwekwa wakfu, na ya sadaka za amani; ambazo BWANA alimwagiza Musa katika mlima wa Sinai, siku hiyo aliyowaagiza wana wa Israeli wamtolee BWANA matoleo yao, huko katika jangwa la Sinai.
Walawi 7:1-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na sheria ya hiyo sadaka ya hatia ni hii; ni takatifu sana. Wataichinja sadaka ya hatia pale pale waichinjapo sadaka ya kuteketezwa; na damu yake atainyunyiza katika madhabahu pande zote. Katika sadaka hiyo atasongeza mafuta yake yote; yaani, mkia wake wenye mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na figo zake mbili, hayo yote atayaondoa; na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kuwa dhabihu kwa BWANA kwa njia ya moto; ni sadaka ya hatia. Kila mtu mume miongoni mwa makuhani atakula katika sadaka hiyo; italiwa katika mahali patakatifu; ni takatifu sana. Kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo, na sadaka ya hatia ni vivyo; sheria yake ni moja; huyo kuhani afanyaye upatanisho kwayo, ndiye atakayekuwa nayo. Tena kuhani atakayesongeza sadaka ya kuteketezwa ya mtu awaye yote, huyo kuhani atatwaa awe nayo ngozi ya huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa aliyemsongeza. Na kila sadaka ya unga iliyookwa mekoni, na yote yaliyoandaliwa chunguni, au kaangoni, yote yatakuwa ya huyo kuhani aliyeyasongeza. Na kila sadaka ya unga, kama umeandaliwa na mafuta, au kama ni mkavu, watautwaa wana wote wa Haruni kuutumia, kila mtu sawasawa. Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa BWANA, ni hii. Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta. Ataleta matoleo yake, pamoja na mikate iliyotiwa chachu, na pamoja na sadaka zake za amani, kwa ajili ya shukrani. Na katika hayo atasongeza kimoja katika kila toleo kiwe sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA; itakuwa ni ya kuhani atakayeinyunyiza hiyo damu ya sadaka za amani. Na hiyo nyama ya sadaka zake za amani zilizochinjwa kwa ajili ya shukrani italiwa siku iyo hiyo ya matoleo yake; asisaze yo yote hata asubuhi. Lakini kwamba hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa; lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto. Tena kama nyama yo yote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake. Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila; lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu cho chote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yo yote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yo yote, ya ng’ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi. Tena mafuta ya mnyama afaye mwenyewe, na mafuta ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, mna ruhusa kuyatumia kwa ajili ya matumizi mengine; lakini msiyale kabisa. Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa BWANA kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake. Tena msiile damu yo yote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote. Mtu ye yote alaye damu, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa BWANA, atamletea BWANA matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani; mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya BWANA. Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe. Mguu wa nyuma wa upande wa kuume mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka katika hizo sadaka zenu za amani. Katika wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kuume kuwa sehemu yake. Kwa maana, hicho kidari cha kutikiswa, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli. Hii ndiyo sehemu ya Haruni, na sehemu ya wanawe, katika kutiwa mafuta kwao, katika hizo dhabihu zisongezwazo kwa BWANA kwa njia ya moto, siku hiyo aliyowaweka ili wamtumikie BWANA katika kazi ya ukuhani; sehemu ambayo BWANA aliagiza wapewe na wana wa Israeli, siku hiyo aliyowatia mafuta. Ni haki yao ya milele katika vizazi vyao vyote. Sheria ya sadaka ya kuteketezwa ni hii, na ya sadaka ya unga, na ya sadaka ya dhambi, na ya sadaka ya hatia, na ya kuwekwa wakfu, na ya sadaka za amani; ambazo BWANA alimwagiza Musa katika mlima wa Sinai, siku hiyo aliyowaagiza wana wa Israeli wamtolee BWANA matoleo yao, huko katika jangwa la Sinai.
Walawi 7:1-38 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana: Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, nayo damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu. Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia, na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani, figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo. Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia. Mwanaume yeyote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu; ni takatifu sana. “ ‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawasawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho. Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuichukua ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake. Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaango itakuwa ya kuhani anayeitoa. Nayo kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au iko kavu, itakuwa ya wana wa Haruni, nayo itagawanywa sawa kati yao. “ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa BWANA: “ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu na iliyopakwa mafuta, na maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta. Pamoja na sadaka yake ya amani ya shukrani, ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu. Ataleta moja ya kila aina ya andazi kuwa sadaka, matoleo kwa BWANA; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani. Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku hiyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote hadi asubuhi. “ ‘Lakini ikiwa sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini chochote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake. Nyama yoyote ya sadaka inayobaki hadi siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto. Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, BWANA hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi. Mtu atakayekula sehemu yake yoyote atahesabiwa hatia. “ ‘Nyama inayogusa chochote kilicho najisi kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu yeyote aliyetakaswa anaweza kuila. Lakini kama mtu yeyote najisi akila nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa BWANA, huyo mtu lazima akatiliwe mbali na watu wake. Kama mtu yeyote akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu chochote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa BWANA, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ngʼombe, kondoo wala mbuzi. Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na wanyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale. Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa BWANA kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. Popote mtakapoishi, kamwe msile damu ya ndege yeyote wala ya mnyama. Mtu yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote aletaye sadaka ya amani kwa BWANA ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa BWANA. Ataleta sadaka kwa mikono yake mwenyewe iliyotolewa kwa BWANA kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Haruni na wanawe. Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo. Mwana wa Haruni atoaye damu na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake. Kutoka kwa sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa, pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Haruni na wanawe kuwa fungu lao la milele kutoka kwa Waisraeli.’ ” Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto, ambazo zilitengwa kwa ajili ya Haruni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu ili kumtumikia BWANA katika kazi ya ukuhani. Siku ile walipopakwa mafuta, BWANA aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la milele kwa vizazi vijavyo. Basi haya ndio masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu, na sadaka ya amani, ambayo BWANA alimpa Musa juu ya Mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa BWANA, katika Jangwa la Sinai.