Walawi 6:8-23
Walawi 6:8-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Mpe Aroni na wanawe maagizo haya: Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuteketezwa. Sadaka ya kuteketezwa itakuwa motoni juu ya madhabahu usiku kucha hadi asubuhi na moto wake uchochewe, usizimike. Kisha kuhani akiwa amevaa vazi lake rasmi la kitani na kaptura yake ya kitani, atachukua majivu ya ile sadaka kutoka madhabahuni na kuyaweka kando ya madhabahu. Halafu baada ya kubadilisha mavazi yake atayapeleka yale majivu nje ya kambi mahali palipo safi. Moto wa madhabahu lazima uendelee kuwaka, na wala usizimwe. Kila siku asubuhi kuhani ataweka kuni kwenye moto huo na juu yake atapanga sadaka ya kuteketezwa, kabla ya kuteketeza mafuta ya sadaka ya amani. Moto utaendelea kuwaka daima juu ya madhabahu bila kuzimishwa kamwe. “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya nafaka. Wazawa wa Aroni ndio walio na uwezo wa kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka hiyo juu ya madhabahu. Mmoja wa makuhani atachukua konzi moja ya unga wa sadaka ya nafaka pamoja na mafuta na ubani wote na kuviteketeza juu ya madhabahu kama sehemu ya ukumbusho; harufu yake itampendeza Mwenyezi-Mungu. Unga uliosalia atakula Aroni na wazawa wake makuhani bila kutiwa chachu. Wataula kwenye mahali patakatifu uani mwa hema la mkutano. Kamwe usiokwe pamoja na chachu. Nimewapa wao sehemu hiyo kutoka sadaka wanazonitolea kwa moto. Ni sadaka takatifu kabisa kama zilivyo sadaka za kuondoa dhambi na za kuondoa hatia. Wazawa wa kiume wa Aroni ndio peke yao wanaoruhusiwa kula sehemu hiyo maana hiyo imetengwa daima kwa ajili yao kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Yeyote atakayezigusa atakuwa mtakatifu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Tangu wakati wa kuwekwa wakfu kwa Aroni na wazawa wake wanapaswa kumtolea Mwenyezi-Mungu kilo moja ya unga laini kwa siku, nusu moja ya unga huo ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni. Unga huo utachanganywa na mafuta na kuokwa; kisha utauleta ukiwa vipandevipande na kumtolea Mwenyezi-Mungu; na harufu ya sadaka yake itampendeza Mungu. Kuhani aliye mzawa wa Aroni ambaye amepakwa mafuta kushika nafasi yake atamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka hiyo; hilo ni agizo la milele. Sadaka yote itateketezwa. Sadaka yoyote ya nafaka iliyotolewa na kuhani itateketezwa yote; haitaliwa kamwe.”
Walawi 6:8-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa na kumwambia, Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hadi asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike. Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu. Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya kambi hata mahali safi. Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike. Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za BWANA, mbele ya madhabahu. Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa BWANA. Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula. Hautaokwa kwa chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia. Kila mwanamume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya BWANA yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu yeyote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu. BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea BWANA, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni. Utaandaliwa kikaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA. Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa BWANA kwa amri ya milele. Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe.
Walawi 6:8-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa na kumwambia, Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike. Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu. Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi. Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike. Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za BWANA, mbele ya madhabahu. Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa BWANA. Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula. Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia. Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya BWANA yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea BWANA, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni. Utaandaliwa kaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA. Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa BWANA kwa amri ya milele. Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe.
Walawi 6:8-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa: “Mpe Haruni na wanawe agizo hili: ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa: Sadaka ya kuteketezwa itabaki kwenye moto juu ya madhabahu usiku kucha, hadi asubuhi, nao moto lazima uwe unaendelea kuwaka juu ya madhabahu. Kisha kuhani atavaa mavazi yake ya kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani mwilini wake, na aondoe majivu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo moto umeteketeza juu ya madhabahu, na kuyaweka kando ya madhabahu. Kisha atayavua mavazi haya na kuvaa mengine, naye achukue yale majivu nje ya kambi na kuyapeleka mahali palipo safi. Moto ulio juu ya madhabahu lazima uwe unaendelea kuwaka; kamwe usizimike. Kila asubuhi kuhani ataongeza kuni na kupanga sadaka ya kuteketezwa juu ya moto, na kuteketeza mafuta ya wanyama wa sadaka za amani juu yake. Moto lazima uendelee kuwaka juu ya madhabahu mfululizo, kamwe usizimike. “ ‘Haya ndio masharti ya sadaka ya nafaka: Wana wa Haruni wataileta mbele za BWANA, mbele za madhabahu. Kuhani atachukua konzi moja ya unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote ulio juu ya sadaka ya nafaka, na kuteketeza sehemu hiyo ya kumbukumbu juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Haruni na wanawe watakula sehemu iliyobaki, lakini italiwa bila kutiwa chachu mahali patakatifu, nao wataila katika ua wa Hema la Kukutania. Kamwe haitaokwa na chachu; nimewapa kama fungu lao la sadaka iliyotolewa kwangu kwa moto. Ni takatifu sana, kama vile ilivyo sadaka ya dhambi na ya hatia. Kila mwanaume mzao wa Haruni aweza kuila. Ni fungu lake milele la sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto kwa vizazi vijavyo. Chochote kinachozigusa kitakuwa kitakatifu.’ ” Tena BWANA akamwambia Musa, “Hii ni sadaka ambayo Haruni na wanawe wanapaswa kuleta kwa BWANA siku atakapopakwa mafuta: sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kama sadaka ya kawaida ya nafaka. Nusu yake ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni. Iandae kwa mafuta kwenye kikaango; ilete ikiwa imechanganywa vizuri, na utoe hiyo sadaka ya nafaka ikiwa imevunjwa vipande vipande kuwa harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Mwanawe atakayeingia mahali pake kama kuhani aliyepakwa mafuta ndiye atakayeiandaa. Ni fungu la milele la BWANA, nalo litateketezwa kabisa. Kila sadaka ya nafaka ya kuhani itateketezwa kabisa; kamwe haitaliwa.”