Walawi 5:1-19
Walawi 5:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kama mtu yeyote akitakiwa kutoa ushahidi kwenye baraza juu ya jambo aliloona au kulisikia naye akakataa kusema kitu, basi, huo ni uovu na atauwajibikia. Au kama mtu yeyote miongoni mwenu amekuwa najisi bila kukusudia kwa kugusa kitu chochote najisi, iwe ni mzoga wa mnyama wa porini au wa kufugwa au wadudu, atakuwa na hatia. Au mtu akigusa chochote kilicho najisi cha binadamu, kiwe kiwacho, ambacho humfanya mtu kuwa najisi, naye hana habari, basi, atakapojua atakuwa na hatia. Au, kama mtu akiapa kufanya chochote kile, chema au kibaya, kama wafanyavyo watu bila kufikiri, atakapojua atakuwa na hatia. Basi, mtu akiwa na hatia kuhusu mambo hayo lazima akiri dhambi yake aliyotenda na kumletea Mwenyezi-Mungu sadaka yake ya kuondoa hatia. Kwa ajili ya dhambi aliyotenda ataleta kondoo jike au mbuzi jike kutoka kundi lake amtoe sadaka kwa ajili ya kuondoa dhambi. Naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake. “Lakini kama hawezi kutoa mwanakondoo wa sadaka ya kuondoa hatia kwa ajili ya dhambi aliyotenda, basi atamletea Mwenyezi-Mungu hua wawili au makinda mawili ya njiwa: Mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Atawaleta kwa kuhani, naye kuhani atamtoa mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi kwa kumkongonyoa shingo yake bila kukichopoa kichwa chake. Sehemu ya damu yake ataipaka pembeni mwa madhabahu na ile nyingine ataimimina chini kwenye tako la madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kisha atamtoa yule wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa kulingana na maagizo. Kuhani atamfanyia huyo mtu upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. “Ikiwa hawezi kutoa hua wawili au makinda mawili ya njiwa kama sadaka yake ya kuondoa dhambi aliyotenda, basi, ataleta unga kilo moja. Lakini hatautia mafuta wala ubani kwani ni sadaka ya kuondoa dhambi. Atamletea kuhani, naye atachukua unga huo konzi moja na kuuteketeza juu ya madhabahu kama sehemu ya ukumbusho, pamoja na sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, naye atasamehewa. Unga unaobaki utakuwa wake kuhani kama ifanyikavyo kuhusu sadaka ya nafaka.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Kama mtu yeyote akikosa kwa kutenda dhambi bila kujua kuhusu kutotoa vitu vitakatifu anavyotolewa Mwenyezi-Mungu, atamletea kondoo dume asiye na dosari kutoka kundi lake. Wewe utapima thamani yake kulingana na kipimo rasmi cha mahali patakatifu. Hiyo ni sadaka ya kuondoa hatia. Zaidi ya hayo, huyo mtu atalipa madhara yote aliyosababisha kuhusu vitu vitakatifu kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani yake na kumpatia kuhani yote. Basi, kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa huyo kondoo dume aliye sadaka ya kuondoa hatia, naye atasamehewa. “Mtu yeyote akitenda dhambi bila kujua, kwa kuvunja amri yoyote ya Mwenyezi-Mungu, yeye ana hatia, na atalipa adhabu ya hatia yake. Atamletea kuhani kondoo dume asiye na dosari kutoka kundi lake akiwa na thamani sawa na ile ya sadaka ya hatia. Na kuhani atamfanyia upatanisho kwa kosa alilofanya, naye atasamehewa. Hiyo ni sadaka ya hatia; yeye ana hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu.”
Walawi 5:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na mtu yeyote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe; au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni mzoga wa mnyama nyikani aliye najisi, au ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au ni mzoga wa mdudu aliye najisi, bila kujua, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake; au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu wowote ambao kwao amepata unajisi, bila kujua, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia; au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lolote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, bila kujua; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo; kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa; naye atamletea BWANA sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake. Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea BWANA hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa. Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamvunja shingo kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili; kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi. Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa. Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi. Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi. Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya BWANA; ndipo atakapomletea BWANA sadaka yake ya hatia, kondoo dume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia; naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa. Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia pia, naye atachukua uovu wake. Naye ataleta kondoo dume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa. Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za BWANA.
Walawi 5:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na mtu awaye yote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe; au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, kama ni mzoga wa mnyama wa nyikani aliye najisi, au kama ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au kama ni mzoga wa mdudu aliye najisi, naye jambo hilo linamfichamania, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake; au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu uwao wote ambao kwa huo amepata unajisi, na jambo hilo linamfichamania, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia; au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo; kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa; naye atamletea BWANA sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake. Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea BWANA hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa. Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamkongonyoa kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili; kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi. Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa. Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi. Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi. Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya BWANA; ndipo atakapomletea BWANA sadaka yake ya hatia, kondoo mume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia; naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa. Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake. Naye ataleta kondoo mume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa. Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za BWANA.
Walawi 5:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“ ‘Ikiwa mtu ametenda dhambi kwa sababu hakusema alipotakiwa kutoa ushahidi hadharani kuhusu jambo aliloona au kujua habari zake, yeye atastahili adhabu. “ ‘Au mtu akitambua kuwa ana hatia, kama vile akigusa kitu chochote ambacho ni najisi, iwe ni mizoga ya wanyama pori walio najisi, au ya wanyama wafugwao walio najisi, au ya viumbe vinavyotambaa ardhini, hata akiwa hana habari, amekuwa najisi na mwenye hatia. “ ‘Au akigusa kitu kilicho kichafu kinachotokana na binadamu, kitu chochote kile kinachoweza kumfanya awe najisi, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia. “ ‘Au kama mtu ameapa kufanya kitu chochote bila kufikiri, kiwe chema au kibaya, kwa vyovyote mtu aweza kuapa bila kujali, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia. “ ‘Mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, ni lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi, na kama adhabu ya dhambi aliyoitenda, ni lazima alete kwa BWANA kondoo jike au mbuzi jike kutoka kundi lake kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake. “ ‘Lakini kama huyo mtu hataweza kumtoa mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda wawili wa njiwa kwa BWANA ikiwa ni adhabu kwa ajili ya dhambi yake: mmoja wa hao ndege kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wa pili kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Atawaleta kwa kuhani, ambaye atamtoa kwanza ndege mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atamvunja shingo na kuacha kichwa chake kikiningʼinia, naye atanyunyiza sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi kwenye pembe za madhabahu. Damu iliyobaki lazima ichuruzwe chini ya madhabahu. Hii ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atamtoa yule ndege wa pili kama sadaka ya kuteketezwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na hivyo kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa. “ ‘Ikiwa basi hawezi kupata hua wawili au makinda wawili wa njiwa, ataleta sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kamwe asiweke mafuta wala uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya dhambi. Atauleta unga kwa kuhani, ambaye atachukua konzi moja kama sehemu ya kumbukumbu na atauteketeza kwenye madhabahu juu ya sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto. Hii ni sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yoyote ya hizo alizotenda, naye atasamehewa. Sadaka iliyobaki itakuwa ya kuhani, kama ilivyokuwa ile sadaka ya nafaka.’ ” BWANA akamwambia Musa: “Mtu anapokiuka na kutenda dhambi pasipo kukusudia kuhusu mojawapo ya mambo matakatifu ya BWANA, huyo mtu ataleta kwa BWANA kama adhabu kondoo dume mmoja kutoka kundi lake, asiye na dosari, na mwenye thamani halisi ya fedha kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Hii ni sadaka ya hatia. Ni lazima alipe kwa yale aliyoshindwa kufanya kuhusu vitu vitakatifu, kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani ile na kuitoa yote kwa kuhani, ambaye atamfanyia upatanisho kwa huyo kondoo dume kama sadaka ya dhambi, naye atasamehewa. “Kama mtu akifanya dhambi, na kutenda yaliyokatazwa katika mojawapo ya amri za BWANA, hata ikiwa hajui, yeye ana hatia na anastahili adhabu. Atamletea kuhani kama sadaka ya hatia kondoo dume kutoka kundi lake, kondoo asiye na dosari na mwenye thamani halisi. Kwa njia hii, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa kosa alilotenda bila kukusudia, naye atasamehewa. Hii ni sadaka ya hatia; amekuwa na hatia kwa kufanya kosa dhidi ya BWANA.”