Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 4:13-31

Walawi 4:13-31 Biblia Habari Njema (BHN)

“Iwapo jumuiya yote nzima ya Israeli imetenda dhambi bila ya kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu mara dhambi hiyo itakapojulikana, jumuiya yote itatoa fahali mchanga awe sadaka ya kuondoa dhambi. Watamleta kwenye hema la mkutano. Wazee wa jumuiya ya watu wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali, kisha atachinjwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yule kuhani aliyeteuliwa rasmi kwa kupakwa mafuta ataleta sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya hema la mkutano. Atachovya kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza mbele ya pazia mara saba, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, sehemu ya damu atazipaka pembe za madhabahu iliyoko katika hema la mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyo karibu na mlango wa hema la mkutano. Mafuta yote ya mnyama huyo atayachukua na kuyateketeza kwenye madhabahu. Kwa hiyo atamfanya fahali huyu kama alivyomfanya yule mwingine wa sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, huyo kuhani atawafanyia watu ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, nao watasamehewa. Kisha atamchukua fahali huyu na kumpeleka nje ya kambi na kumteketeza kwa moto kama alivyomfanya yule mwingine. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi ya jumuiya. “Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia, mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha beberu na kumchinjia mahali wanapochinjia sadaka za kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka. Mafuta yote ya beberu huyo atayateketeza madhabahuni, kama afanyavyo na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa hiyo kuhani atamfanyia mtawala ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. “Kama mtu wa kawaida ametenda dhambi bila kukusudia, kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu na hivyo akawa na hatia, mara atakapojulishwa kuwa ametenda dhambi, ataleta sadaka ya mbuzi jike asiye na dosari kwa ajili ya kuondoa dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu iliyobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa.

Shirikisha
Soma Walawi 4

Walawi 4:13-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi bila kukusudia, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na BWANA, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia; hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng'ombe dume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania. Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng'ombe mbele za BWANA; kisha ng'ombe atachinjwa mbele za BWANA. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng'ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania; kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za BWANA, mbele ya pazia mara saba. Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za BWANA, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania. Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu. Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng'ombe; kama alivyomfanyia huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu hivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua huyo ng'ombe nje ya kambi, na kumteketeza vile vile kama alivyomteketeza ng'ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano. Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lolote kati ya hayo ambayo BWANA, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi dume asiye na dosari awe matoleo yake; kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za BWANA; ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atatwaa baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza. Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. Na mtu yeyote kati ya watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lolote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi wa kike mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa baadhi ya hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.

Shirikisha
Soma Walawi 4

Walawi 4:13-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na BWANA, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia; hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng’ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania. Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng’ombe mbele za BWANA; kisha ng’ombe atachinjwa mbele za BWANA. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng’ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania; kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za BWANA, mbele ya pazia mara saba. Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za BWANA, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania. Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu. Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng’ombe; kama alivyomfanyia huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua huyo ng’ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng’ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano. Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo BWANA, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu; kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za BWANA; ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atatwaa katika damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza. Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.

Shirikisha
Soma Walawi 4

Walawi 4:13-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“ ‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya BWANA, hata kama jumuiya hawafahamu jambo hilo, wana hatia. Wanapotambua dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko walete fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi, na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania. Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali mbele za BWANA, naye huyo fahali atachinjwa mbele za BWANA. Kisha kuhani aliyepakwa mafuta ataingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania. Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za BWANA mbele ya hilo pazia. Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za BWANA katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania. Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu, naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya. “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya BWANA Mungu wake, ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za BWANA. Hii ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa. “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya BWANA, yeye ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka. Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.

Shirikisha
Soma Walawi 4