Walawi 23:26-32
Walawi 23:26-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni siku ya upatanisho. Siku hiyo ni siku ya kuwa na mkutano mtakatifu. Mtafunga na kutoa sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Msifanye kazi zenu zozote za kawaida siku hiyo. Siku hiyo ni siku ya upatanisho, siku ya kuwafanyieni upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtu yeyote asiyefunga siku hiyo ni lazima atengwe mbali na watu wake. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo nitamwangamiza miongoni mwa watu wake. Msifanye kazi: Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu, na katika makao yenu yote. Siku hiyo, itakuwa kwenu Sabato ya mapumziko rasmi na mtafunga. Siku ya Sabato ni siku ya kumi ya mwezi huo tangu jioni hadi jioni inayofuata.”
Walawi 23:26-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtajinyima; na mtatoa sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Na msifanye kazi yoyote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu. Kwa kuwa mtu yeyote asiyejinyima siku iyo hiyo, atatengwa na watu wake. Na mtu yeyote afanyaye kazi ya namna yoyote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake. Msifanye kazi ya namna yoyote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote. Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtajinyima; siku ya tisa ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hadi jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
Walawi 23:26-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu. Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake. Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake. Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote. Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
Walawi 23:26-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa, “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa BWANA. Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za BWANA Mungu wenu. Mtu ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. Mtu atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi. Ni Sabato ya mapumziko kwenu, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”