Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 23:1-44

Walawi 23:1-44 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Katika sikukuu zangu mimi Mwenyezi-Mungu ambazo zimepangwa mtakuwa na mkutano mtakatifu. Sikukuu ambazo nimepanga ni hizi: Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote. “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa. “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapoingia katika nchi ambayo ninawapeni mkavuna mazao yake, mtamletea kuhani mganda wa mavuno ya kwanza. Kuhani atafanya nayo ishara ya kunitolea siku inayofuata siku ya Sabato ili mpate kukubaliwa. Siku hiyo mnapofanya ishara ya kutoa huo mganda mbele yangu mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya mwanakondoo dume wa mwaka mmoja asiye na dosari. Pamoja na sadaka hiyo, mtatoa sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta ambayo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto, na harufu yake itanipendeza. Sadaka yake ya kinywaji ni lita moja ya divai. Kabla ya siku hiyo ya kuniletea mimi Mungu wenu sadaka hiyo, hamruhusiwi kula mazao ya kwanza ya mavuno yenu, yawe mabichi, yamekaangwa au yemeokwa kuwa mikate. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu mahali popote mtakapoishi. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku ile inayofuata Sabato ile ambapo mtaleta mganda wa sadaka ya kunitolea kwa ishara mimi Mwenyezi-Mungu. Mnamo siku ya hamsini, siku ya pili ya Sabato ya saba, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka mpya. Kila jamaa italeta mikate miwili ya sadaka ya kutoa kwa ishara mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Kila mkate ni lazima uwe umetengenezwa kwa kilo mbili za unga laini uliotiwa chachu; na huo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu ukiwa ni matoleo ya malimbuko yenu. Pamoja na hayo, mtatoa wanakondoo saba wa mwaka mmoja, fahali mchanga mmoja, na kondoo madume wawili. Wanyama hao watakuwa sadaka ya kuteketezwa pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji. Harufu ya sadaka hizi itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Mtatoa beberu mmoja wa sadaka ya kuondoa dhambi na wanakondoo madume wawili wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka za amani. Kuhani atavipitisha mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu viwe sadaka ya kutoa kwa ishara pamoja na mkate wa mavuno ya kwanza na wale wanakondoo wawili. Vitu hivyo ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu navyo vitakuwa kwa matumizi ya kuhani tu. Siku hiyohiyo mtatoa ilani ya mkutano mtakatifu; msifanye kazi. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu. “Unapovuna mavuno yako shambani, kamwe usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba lako wala usirudi nyuma kukusanya masalio. Utawaachia hayo maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie watu wa Israeli hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtaadhimisha siku ya mapumziko rasmi, siku ya ukumbusho itakayotangazwa kwa mlio wa tarumbeta na kufanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi siku hiyo na ni lazima mnitolee mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni siku ya upatanisho. Siku hiyo ni siku ya kuwa na mkutano mtakatifu. Mtafunga na kutoa sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Msifanye kazi zenu zozote za kawaida siku hiyo. Siku hiyo ni siku ya upatanisho, siku ya kuwafanyieni upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtu yeyote asiyefunga siku hiyo ni lazima atengwe mbali na watu wake. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo nitamwangamiza miongoni mwa watu wake. Msifanye kazi: Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu, na katika makao yenu yote. Siku hiyo, itakuwa kwenu Sabato ya mapumziko rasmi na mtafunga. Siku ya Sabato ni siku ya kumi ya mwezi huo tangu jioni hadi jioni inayofuata.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Tangu siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. Hiyo ni sikukuu ya Mwenyezi-Mungu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtakuwa na mkutano mtakatifu na msifanye kazi. Kwa muda wa siku saba mtatoa sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Siku ya nane mtakuwa na mkutano mkubwa na kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa. Mkutano huo ni mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. “Hizo ndizo sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa ambazo mtatoa ilani kuwe na mkutano mtakatifu wa kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zitolewazo kwa moto, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji, kila moja katika siku yake maalumu. Sadaka hizo ni pamoja na zile mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu siku ya Sabato kama vile pia sadaka zenu za kawaida, sadaka za kutimiza nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu. “Baada ya kuvuna mashamba yenu mtafanya sikukuu kwa muda wa siku saba, tangu siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba. Siku ya kwanza itakuwa siku ya mapumziko na hata siku ya nane. Katika siku ya kwanza mtachukua matunda ya miti yenu mizuri, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi na matawi ya miti iotayo kandokando ya mto, nanyi mtafanya sherehe mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kwa siku saba. Kila mwaka ni lazima kuadhimisha sikukuu hii kwa muda wa siku saba kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu. Mtaifanya katika mwezi wa saba. Kwa muda wa siku saba mtaishi katika vibanda. Wakazi wote wa Israeli wataishi katika vibanda wakati huo. Jambo hilo litavijulisha vizazi vyenu kuwa nilipowatoa babu zenu nchini Misri, niliwafanya waishi katika vibanda. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Mose akawatangazia Waisraeli sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa.

Shirikisha
Soma Walawi 23

Walawi 23:1-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayatangaza kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni Pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yoyote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu; naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa. Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume asiye na dosari wa mwaka wa kwanza, awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini. Nanyi msile mkate, bisi, au masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hadi mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote. Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsogezea BWANA sadaka ya unga mpya. Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA. Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, wasio na dosari, wa mwaka wa kwanza, na ng'ombe dume mmoja, na kondoo wawili wa kiume; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Nanyi mtasongeza mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili wa kiume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani. Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa BWANA, wawe wa huyo kuhani. Nanyi mtatangaza suku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yoyote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu. Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu. Msifanye kazi yoyote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtajinyima; na mtatoa sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Na msifanye kazi yoyote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu. Kwa kuwa mtu yeyote asiyejinyima siku iyo hiyo, atatengwa na watu wake. Na mtu yeyote afanyaye kazi ya namna yoyote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake. Msifanye kazi ya namna yoyote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote. Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtajinyima; siku ya tisa ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hadi jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa BWANA. Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Mtamsogezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamtolea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Sikukuu za BWANA ni hizi, ambazo mtazipiga mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee BWANA sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake; zaidi ya hizo Sabato za BWANA, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa BWANA. Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtakapoyachuma mavuno ya nchi, mtasherehekea sikukuu ya BWANA kwa muda wa siku saba; siku ya kwanza na ya nane zitakuwa za kustarehe kabisa. Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, muda wa siku saba. Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa BWANA muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba. Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazaliwa wote wa Israeli watakaa katika vibanda; ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwafanya wana wa Israeli kukaa katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA Mungu wenu. Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 23

Walawi 23:1-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu; naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa. Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini. Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote. Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka ya unga mpya. Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA. Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng’ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani. Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa BWANA, wawe wa huyo kuhani. Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu. Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu. Msifanye kazi yo yote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto. Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu. Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake. Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake. Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote. Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa BWANA. Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. Sikukuu za BWANA ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee BWANA sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake; zaidi ya hizo Sabato za BWANA, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa BWANA. Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya BWANA muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa. Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, muda wa siku saba. Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa BWANA muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba. Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda; ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA Mungu wenu. Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 23

Walawi 23:1-44 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akamwambia Musa, “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu. “ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa BWANA. “ ‘Hizi ni sikukuu za BWANA zilizoamriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamriwa: Pasaka ya BWANA huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza, Sikukuu ya BWANA ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Kwa siku saba mtamletea BWANA sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi nitakayowapa na kuvuna mazao ya nchi hiyo, leteni kwa kuhani mganda wa nafaka ya kwanza mtakayovuna. Naye atauinua huo mganda mbele za BWANA ili ukubaliwe kwa niaba yenu; kuhani ataupunga siku inayofuata Sabato. Siku hiyo mtakapoinua huo mganda, lazima mtoe kwa BWANA dhabihu ya kuteketezwa kwa moto ya mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, pamoja na sadaka yake ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa kuteketezwa kwa moto; hii itakuwa sadaka iliyo harufu nzuri ya kupendeza, na sadaka yake ya kinywaji ya robo ya hini ya divai. Kamwe msile mkate wowote, au nafaka iliyokaangwa au nafaka mpya, hadi siku ile mtakayomletea Mungu wenu sadaka hii. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi. “ ‘Tangu siku ile iliyofuata Sabato, siku mliyotoa sadaka ya mganda wa kuinuliwa, hesabuni majuma saba kamili. Mtahesabu siku hamsini hadi siku inayofuata Sabato ya saba, ndipo mtatoa sadaka ya nafaka mpya kwa BWANA. Kutoka popote mnapoishi, mtaleta mikate miwili iliyotengenezwa kwa sehemu mbili za kumi ya efa moja ya unga laini, uliookwa kwa chachu, kuwa sadaka ya kuinuliwa ya malimbuko kwa BWANA. Toeni pamoja na hiyo mikate wana-kondoo saba, kila mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari, na fahali mchanga, na kondoo dume wawili. Watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa BWANA, pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, sadaka iliyotolewa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Kisha toeni dhabihu ya beberu mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili, kila mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya amani. Kuhani atawainua hao wana-kondoo wawili mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa, pamoja na mkate wa malimbuko. Ni sadaka takatifu kwa BWANA kwa ajili ya kuhani. Siku hiyo hiyo mtatangaza kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mtakapoishi. “ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu, au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na Sabato ya mapumziko, kusanyiko takatifu la ukumbusho litakaloadhimishwa kwa kupiga tarumbeta. Msifanye kazi zenu zozote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa BWANA iliyoteketezwa kwa moto.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa BWANA. Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za BWANA Mungu wenu. Mtu ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. Mtu atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi. Ni Sabato ya mapumziko kwenu, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.” BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba kwa BWANA. Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida. Kwa siku saba toeni sadaka kwa BWANA za kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu, na kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa BWANA. Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida. (“ ‘Hizi ni sikukuu za BWANA zilizoamriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa BWANA za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku. Sadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za BWANA, na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya chochote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa BWANA.) “ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa BWANA kwa siku saba; siku ya kwanza ni Sabato ya mapumziko, na pia siku ya nane ni Sabato ya mapumziko. Siku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za BWANA Mungu wenu kwa siku saba. Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa BWANA kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni mwezi wa saba. Mtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda, ili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” Kwa hiyo Musa akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamriwa na BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 23