Walawi 19:19-37
Walawi 19:19-37 Biblia Habari Njema (BHN)
“Yakupasa kuyashika masharti yangu. Usiiache mifugo yako ipandwe na wanyama wa aina nyingine. Shambani mwako usipande mbegu za aina mbili. Usivae vazi lililofumwa kwa aina mbili za nguo. “Mwanamume akilala na mwanamke mtumwa ambaye ameposwa na mwanamume mwingine, lakini bado hajakombolewa wala kupewa uhuru, uchunguzi ufanywe. Lakini wasiuawe kwa sababu mwanamke huyo hakuwa bado huru. Mwanamume huyo ataleta mbele ya hema la mkutano sadaka yake ya kondoo dume ya kuondoa hatia na kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa kutumia kondoo huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya dhambi aliyotenda; naye atasamehewa dhambi hiyo aliyotenda. “Mtakapofika katika nchi ya Kanaani na kupanda aina zote za miti ya matunda, matunda hayo hamtayala; hamtaruhusiwa kuyala kwa muda wa miaka mitatu. Mnamo mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa matakatifu, yatatolewa kuwa sadaka ya sifa, kwa Mwenyezi-Mungu. Lakini matunda ya kuanzia mwaka wa tano hayo mnaweza kula, na mavuno yenu yataongezeka. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msile nyama yoyote yenye damu. Msipige bao wala kufanya uchawi. Nywele zenu msizikate pembeni wala kunyoa ndevu zenu. Msijitie alama zozote mwilini mwenu kwa ajili ya kuomboleza au kujikatakata mwilini au kujichanja chale. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimchafue binti yako kwa kumfanya kahaba, nchi nzima isije ikaangukia katika ukahaba na hivyo kujaa uovu. Mtazishika Sabato zangu na kupaheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Msiwaendee waaguzi wa mizimu wala wachawi ili kuwaomba wawaagulie na hivyo mkajitia najisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Uwapo mbele ya mzee ni lazima usimame ili kumpa heshima yake; nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Kama kuna mgeni katika nchi yako usimtendee vibaya. Huyo mgeni anayekaa nawe atakuwa kwako kama mwenyeji nawe utampenda kama unavyojipenda mwenyewe, kwa kuwa nawe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Usikose kamwe kuamua kwa haki kuhusu vipimo vya urefu, uzito na ujazo. Ni lazima mtumie mizani halali, na vipimo vilivyo halali. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. Ni lazima kuyashika na kuyatekeleza masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
Walawi 19:19-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja. Tena mtu yeyote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mwanamume mwingine, wala hakukombolewa kwa lolote, wala hakupewa uhuru wake; watachunguzwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru. Na huyo mwanamume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa BWANA, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo dume kwa hiyo sadaka ya hatia. Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia mbele za BWANA, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya. Nanyi mtakapoingia katika nchi ile, na kupanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama yaliyotakazwa; kwa muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama katazo; matunda yake hayataliwa. Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa BWANA shukrani. Na katika mwaka wa tano mtakula matunda yake, ili ipate kuwapa mavuno yake; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msile kitu chochote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. Msichanje chale yoyote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA. Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu. Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA. Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi BWANA. Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni aishiye pamoja nawe atakuwa kama mzaliwa kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo. Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi BWANA.
Walawi 19:19-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja. Tena mtu ye yote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mume, wala hakukombolewa kwa lo lote, wala hakupewa uhuru; wataadhibiwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru. Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa BWANA, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia. Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za BWANA, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya. Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa. Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa BWANA shukrani. Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA. Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu. Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA. Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi BWANA. Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo. Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi BWANA.
Walawi 19:19-37 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“ ‘Mtazishika amri zangu. “ ‘Usiwaache mifugo wako wakazaana na wa aina tofauti. “ ‘Usipande mbegu za aina mbili katika shamba lako. “ ‘Usivae vazi lililofumwa kwa nyuzi za aina mbili tofauti. “ ‘Kama mwanaume anakutana kimwili na mjakazi aliyeposwa na mwanaume mwingine, ambaye hajakombolewa wala hajapewa uhuru, lazima iwepo adhabu inayofaa. Hata hivyo hawatauawa, kwa sababu msichana alikuwa bado hajaachwa huru. Lakini huyo mtu lazima alete kondoo dume kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa ajili ya sadaka ya hatia kwa BWANA. Kupitia kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA kwa ajili ya dhambi aliyotenda, naye atasamehewa dhambi yake. “ ‘Mtakapoingia katika hiyo nchi na kupanda aina yoyote ya mti wa matunda, hesabuni matunda yake kama yaliyokatazwa. Kwa miaka mitatu mtayahesabu kwamba yamekatazwa; hayaruhusiwi kuliwa. Katika mwaka wa nne matunda yote ya mti huo yatakuwa matakatifu, sadaka ya sifa kwa BWANA. Bali katika mwaka wa tano mnaweza kula matunda ya mti huo. Kwa njia hii mavuno yenu yataongezewa. Mimi ndimi BWANA Mungu wako. “ ‘Msile nyama yoyote yenye damu ndani yake. “ ‘Msifanye uaguzi wala uchawi. “ ‘Msikate nywele za kichwa denge, wala kunyoa pembe za ndevu zenu. “ ‘Msichanje chale miili yenu kwa ajili ya mfu, wala msijichore alama juu ya miili yenu. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Usimdhalilishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo nchi itageukia ukahaba na kujaa uovu. “ ‘Shika Sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Msiende kwa waaguzi, wala msitafute wapunga pepo, kwa maana watawanajisi. Mimi ndimi BWANA Mungu wako. “ ‘Ukiwa mbele ya mzee, simama ili kuonesha heshima kwa wazee, nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase. Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi BWANA Mungu wako. “ ‘Usitumie vipimo vya udanganyifu unapopima urefu, kupima uzito, wala kupima wingi. Tumia mizani halali, mawe ya kupimia uzito halali, efa halali, na hini halali. Mimi ndimi BWANA Mungu wako, ambaye alikutoa katika nchi ya Misri. “ ‘Shika amri zangu zote na sheria zangu zote, nawe uzifuate. Mimi ndimi BWANA.’ ”